Friday, July 27, 2012

YANGA YAICHAPA APR 1 -0, KUCHEZA NA AZAM FAINALI

Kikosi chaYoung Africans kilichocheza Nusu Fainali dhidi ya APR na kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Hamis Kiiza'Diego' wa kwanza kulia akishangilia bao alilofunga katika mchezo dhidi ya APR, anayefuatia ni Godfrey Taita, Haruna Niyonzima na Rashid Gumbo
Mabingwa watetezi wa kombe la klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, timu ya Young Africans Sports Club imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo siku ya jumamosi, baada ya kuichapa APR kutoka Rwanda kwa bao 1- 0, katika mchezo mkali wa nusu fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Mchezo huo ambao ulianza majira ya saa 10 kamili jioni, ulikuwa ni mkali na wa kuvutia muda wote wa mchezo, kitu kilichopelekea kumalizika kwa dakika 90 timu zote zikiwa sare ya kutofungana bao, hali iliyopelekea kunongezwa dakika 30 za muda wa ziada.

APR amabo waliingia uwanjani kwa nia ya kulipiza kisasi kwa Young Africans kufuatia kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa awali hatua ya makundi, waliuanza mchezo kwa kasi na kufanya mashambulizi ya kushitukiza, lakini umahiri wa mlinda mlango Ally Mustapha 'Barthez' ulikuwa kikwazo kwako.

Dakika ya 26 ya mchezo, Young Africans ilipata pigo baada ya mlinzi wake wa upande wa kulia Juma Abdul kukanyagwa vibaya mguuni na mchezaji wa APR Tuyizere Donatien hali iliyopelekea mchezaji huyo kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Shamte Ally.

Kuona hivyo APR waliamua kupitia upande wa kulia wa Young Africans ambapo dakika ya 26 na dakika ya 38 Godfrey Taita na Shamte Ally walionyeshwa kadi za njano mwamuzi, kwa kuwachezea vibaya wachezaji wa APR.

Mpaka mpira unakwenda mapumziko, timu zote zilikuwa hazijafunagana zaidi ya kushambuliana kwa zamu. mwamuzi wa mchezo huo pia alishindwa kuumudu mchezo kwani alishinbdwa kuonyesha kadi kwa wachezaji wa APR kitu kilichofanya mashabiki kupiga kelele nyingi na kumzomea. 

Kipindi cha pili cha mchezo, Young Africans iilionekana kubadilika sana, kwani iliweza kumiliki vizuri mpira na sehemu ya kiungo, hali iliyowapelekea wachezaji wa APR wengi kurudi kukabia nyuma ya mstari wa katikakati.

Said Bahanunzi alikosa bao la wazi dakika ya 66, akishindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Hamis Kiiza na Bahnunzi kushindwa kumchambua mlinda mlango wa APR Jean Claude Ndoli aliyepangua shuti lake na kuwa kona.

Young Africans iliendelea kukitawala kipindi cha pili, dakika ya 86 ilifanya mabadiliko ya kumtoa Shamte Ally na kumuingiza Rashid Gumbo ambaye aliongeza uhai katika nafasi ya kiungo.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika timu zote zilikuwa sare ya kutofungana, Young Africans 0 - 0 APR.

Mwamuzi aliongeza dakika 30 za nyongeza, ambapo timu zote zilainza kusaka bao la mapema ili kuweza kuwasogeza hatua ya fainali, Mbuyu Twite alimchezea vibaya Rashid Gumbo lakini katika haliya kushangaza mwamuzi hakumpa kadi yoyote hali iliyopelekea wachezaji wa Young Africans kuja juu,Hamis Kiiza 'Diego' aliipatia Young Africans bao la kwanza na la ushindi katika dakika ya 100 ya mchezo akimalizia krosi safi iliyopigwa Haruna Niyonzima na Kiiza kufunga kwa bao hilo maridadi kwa kifua.

Kuona hivyo APR walianza kucheza mchezo wa kuwakwatua wachezaji wa Young Africans, hali iliyoleta majibizano na mwamuzi ambapo dakika ya 103, mwamuzi alimuonyesha kadi nyekundu mlinzi wa kulia wa Young Africans Godfrey Taita.

Mara baada ya kuona wako pungufu , Young Africans ilirudi nyuma kujipanga na kucheza mchezo wa kushitukiza huku ikilinda bao lake hilo.

Mpaka dakika 120 za mchezo zinamalizika, Young Africans iliibuka na ushindi wa bao 1-0 , hivyo kukata tiketi ya kucheza FAINALI na Azam FC siku ya jumamosi, fainali itakayofanyika majira ya saa 10 kamili jioini Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Saa 8 mchana kutakuwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya APR na AS Vita.

Young Africans : 1.Barhtez, 2.J. Abdul/Shamte/Gumbo, 3.Oscar, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Chuji, 7.Taita , 8.Niyonzima, 9.Bahanunzi, 10.Kiiza, 11.Luhende

APR: 1.Ndoli, 2.Ngabo. 3.Tuyizere, 4.Twite, 5.Bagoole, 6.Iranzi, 7.Preus, 8.Mugiranenza, 9.Karekezi, 10.Wagaluka, 11.Ndikumana.

No comments:

Post a Comment

only comments that are benefial for this blog is allowed