Uongozi wa klabu ya Young Africans Sports Club pamoja na benchi lake la ufundi, umewapa mapumziko ya wiki moja wachezaji wake wote kusheherekea Ubingwa wa Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kombe la Kagame walioutwaa siku chache zilizopita.
Akiongea na tovuti ya klabu www.youngafricans.co.tz kocha mkuu wa Young Africans, Mbeligiji Tom Saintfiet amesema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mashindano na kwa hakika kujituma kwao na kusikilliza maelekezo yake ndio kilichochangia mafanikio hayo.
Young Africans ilifanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara ya tano (5), ikiwa pia ni mara ya pili mfululizo baada ya kulitwaa kombe hilo mwaka 2011.
Katika mchezo wa fainali Young Africans iliifunga timu ya Azam FC mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya Hamis Kiiza 'Diego' aliyefunga dakika ya 44 na Said Bahanunzi aliyefunga dakika ya 92 ya mchezo.
Kocha Tom Saintfiet amesema vijana wake wameanza mapumziko hayo toka siku ya jumamosi baada ya kutwaa Ubingwa na wanatakiwa wote kuwepo siku ya ijumaa tarehe 3/08/2012 asubuhi saa 3 katika mazoezi.
Mazoezi yataendelea kufanyika katika Uwanja wa shule ya Sekondari Loyola mpaka itakapoanza ligi kuu ya Vodacom Septemba Mosi kama hakutakuwa na mabadiliko ya ratiba.
Kwa upande wa Uongozi, katibu mkuu wa Young Africans Mwesigwa Selestine amesema timu yake haitashiriki mashindano ya ABC Bank super8 kutokana na mashindano hayo kuja ghafla wakati kocha tayari alikuwa ameshatoa programu yake ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.
Kwa maana hiyo Young Africans haitashiriki mashindano na itaendelea na programu ya mwalimu mpaka hapo msimu mpya wa ligi kuu utakapoanza Septemba mosi.
Pia Uongozi unawapongeza wapenzi, washabiki na wanachama wa Young Africans kwa moyo wao safi, kuishangilia timu yao toka mwanzo wa mashindano, kitu ambacho kiliwapa hamasa wachezaji kucheza na kujituma ili kuwapa furaha washabiki wao.
No comments:
Post a Comment
only comments that are benefial for this blog is allowed