Monday, August 06, 2012

HABARI KUTOKA TFF

Tenga Kufungua Kozi Ya Uongozi Ya FIFA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anatarajia kufungua Kozi ya Uongozi na Utawala ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inayoanza kesho (Agosti 6 mwaka huu) Msimbazi Center jijini Dar es Salaam.

Kozi hiyo itakayokuwa na washiriki zaidi ya 30 itamalizika Agosti 11 mwaka huu na itaendeshwa na Wakufunzi kutoka FIFA na itafunguliwa saa 3 asubuhi. Wakufunzi hao ni Barry Rukoro anayetoka Namibia, Henry Tandau (Tanzania) na Senka Kanyenvu (Botswana).

Baadhi ya washiriki wa kozi hiyo ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA Amani Makungu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy Kiondo, Stanley Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud Mvella.

Wengine ni Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, wenyeviti wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi), Dodoma (Nassoro Kipenzi) na Pascal Kihanga (Morogoro).

Makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent Majiri), Morogoro (Hamisi Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya) na Dodoma (Stuart Masima). Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Hilal na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.

Washiriki wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, Ofisa Habari, Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy Kabwe na Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba.

Wengine ni Ofisa Sheria wa TFF, Neema Lucumay, Ofisa wa Mpira wa Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma (Mpira wa miguu wa wanawake) na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

only comments that are benefial for this blog is allowed