
LONDON, ENGLAND
MARIO Balotelli (22), ameamua kusaka ushauri wa mchungaji wa kanisa ili asitimuliwe kutoka Manchester City baada ya kugombana na kocha wake Roberto Mancini.
Balotelli amekutana mara nyingi na mchungaji huyo, ambaye ameajirwa na Manchester City.
Amechukua hatua hiyo baada ya kukunjana mashati na kocha, kitu ambacho kinaweza kumfukuzisha kutoka katika klabu hiyo.
Balotelli alikunjana na kocha wake baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo wiki hii.
Mtaliano huyo ameonana na Mchungaji Peter Horlock mwenye umri wa miaka ya 36 mara kibao katika siku za hivi karibuni.
Manchester City ni klabu ambayo huangalia wachezaji wake vizuri na ndiyo maana imemwajiri Mchungaji Horlock, ambaye alitaarifiwa kuhusu tukio hilo lilitokea katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.
Ugomvi unadaiwa ulianza wakati Mancini alipomwamuru Balotelli kuondoka uwanjani baada ya kumchezea rafu mbaya Scott Sinclair mazoezini.
Baada ya hapo, Balotelli alianza kumzodoa Sinclair kitu ambacho kilimkasirisha Mancini, ambaye alimtaka atoke uwanjani.
Balotelli aligoma kutoka uwanjani na Mancini aliamua kumshika shingoni na kumtoa kwa nguvu.
Mshambuliahi huyo aligoma kutoka naye akamshika kocha wake.
Makocha wasaidizi, Brian Kidd na Massimo Battara waliingilia kali kujaribu kutuliza ugomvi lakini Mancini bado alitaka kumvaa Balotelli.
Tukio hilo lilipigwa picha na mpita njia katika eneo hilo.
Baada ya kitendo hicho, Balotelli aliondoka na gari lake aina ya Bentley.
Kuna uwezekano akapigwa faini kubwa baada ya kuonyesha kiburi kwa kocha.
Baada ya tukio hilo, Balotelli ana nafasi finyu ya kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Watford leo Jumamosi.
Balotelli amekuwa na kasheshe katika klabu hiyo tangu alipojiunga nayo.
Balotelli anamtegemea Mchungaji Horlock amsaidie.
Mancini, ambaye ni Mkatoliki inadaiwa naye amekutana na mchungaji huyo, ambaye ana kazi ya kuwashauri wachezaji wanaofuata dini ya Kikristo.
No comments:
Post a Comment
only comments that are benefial for this blog is allowed