Tuesday, February 05, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF



Tiketi Stars, Cameroon Kuanza Kuuzwa Leo Feb 5
Tiketi kwa ajili ya pambano la kimataifa la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) zinaanza kuuzwa leo (Febaruari 5 mwaka huu) katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Viingilio katika pambano hilo litakalochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni ni sh. 5,000 (viti vya kijani), sh. 7,000 (viti vya bluu), sh. 10,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na sh. 30,000 VIP A.

Vituo vitakavyouzwa tiketi hizo kuanzia saa 2 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Oilcom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.

Vilevile tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi, na milango itafunguliwa saa 8 kamili mchana.

Wakati huo huo, kundi la kwanza na la pili la wachezaji wa Cameroon tayari limetua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Cameroon chini ya Kocha Jean Paul Akono itafanya mazoezi kesho saa 11 jioni Uwanja wa Taifa. Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager yenyewe itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa leo saa 11 jioni.

Mkutano Wa Makocha Wa Stars Na Cameroon Na Waandishi Wa Habari
Makocha wa timu za Tanzania, Kim Pousen na Cameroon, Jean Paul Akono na manahodha wao Juma Kaseja Juma na Samuel Eto'o Fils leo (Februari 5 mwaka huu) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia pambano la keshokutwa. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

only comments that are benefial for this blog is allowed