
Shirikisho la soka
nchini Tanzania (TFF) limethibitisha kwa Shirikisho la Vyama vya Mpira
wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kuwa timu ya taifa ya
wanawake ya Tanzania itashiriki michuano ya kwanza ya Kombe la Chalenji
kwa wanawake itakayofanyika kuanzia Septemba 11, 2016 hadi Septemba 20,
2016 kwa kushirikisha nchi saba wanachama wa shirikisho hilo.
Kwa
mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na Tanzania
ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za
Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na
Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar
pamoja na mwenyeji Uganda.
Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016.
Rwanda
na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata
utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na
Kenya.
Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na
Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar
itacheza na Uganda.
Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.
Nusu
fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20,
2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.
Mashindano
ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo
linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka ya wanawake
kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Tanzania inatarajiwa
kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani
kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa
safari ya Uganda.
SOURCE:http://www.bbc.com/swahili
No comments:
Post a Comment
only comments that are benefial for this blog is allowed